Monday, 21 January 2013

Raisi Akutana na Watanzania Ufaransa
Akiwa katika ziara kiserikali nchini Ufaransa, raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Jakaya Mrisho Kikwete amekutana na watanzania waishio Ufaransa Jumapili jioni tarehe 20 Januari katika ukumbi wa Hoteli ya Le Meurice mjini Paris.

Mheshimiwa Raisi alitumia fursa hii kushukuru Jumuiya ya Watanzania Ufaransa kwa juhudi zao za kuitangaza Tanzania nchini Ufaransa. Mh Kikwete alieleza jinsi ambavyo serikali inajizatiti katika kukuza uchumi, na kuhakikisha kuwa wananchi wengi wanapata huduma muhimu kama afya, maji safi, barabara, elimu na umeme.

Akizungumzia hali ya siasa, alisema nchi ni salama na hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi. Chokochoko za kisiasa ni sehemu ya maisha ya kila siku. Alisema mchakato wa kupata katiba mpya unaendelea na wananchi wanaendelea kutoa maoni yao.

Akijibu hotuba ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania Ufaransa, Mama Delly Makombe, Rais Kikwete alisema kwamba serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha ununuzi wa nyumba kwa ajili ya ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa. Raisi aliahidi kuendelea kuenzi na kusaidia kazi nzuri inayofanywa na Jumuiya ya Watanzania na Ubalozi.

Katika ziara hiyo, Mh Kikwete aliongozana na Mama Salma Kikwete, Mawaziri: Mh Bernard Membe (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), Mh John Magufuli (Waziri wa Ujenzi), Mh Prof. Sospeter Muhongo (Waziri wa Nishati na Madini) na Mh Said Ali Mbarouk (Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar).

No comments: