Wednesday, 22 January 2014

Chadema kutikisa nchi; Helikopta kurushwa nchi nzima

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuanzia leo, kinarusha helkopta tatu kwa siku 14 mfululizo, katika  kutekeleza kampeni iliyopewa jina la Operesheni Pamoja Daima (ODB) itakayoendeshwa katika mikoa yote nchini.
Ziara hiyo inaanzia katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Ruvuma, huku viongozi wa chama hicho wakijigawa katika makundi sita; matatu yakitumia helkopta na matatu yatawafikia wananchi kwa kutumia usafiri wa magari.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa, lengo la operesheni hiyo ni kukiimarisha chama hicho na kuwafumbua macho wananchi kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.
“Tumejigawa katika makundi sita na makundi matatu kati ya hayo yatatumia helikopta kila moja, makundi mengine yatawafikia wananchi kwa misafara ya ardhini,” alisema Mbowe na kuongeza;
“Viongozi wakuu wa chama, wabunge, wenyeviti wa mikoa, wilaya, majimbo na kanda kila mmoja atashiriki kwa nafasi yake katika operesheni hii. Tutafanya mikutano kwa wiki mbili, ila tunaweza kuongeza wiki nyingine moja.”
Alisema chama hicho kimejipanga kuwafikia wananchi wengi kadri itakavyowezekana, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wake wa ndani kuanzia ngazi ya mashina, uchaguzi mdogo wa madiwani katika Kata 27 nchini utakaofanyika Februari 9, mwaka huu pamoja na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Naomba tueleweke, katika hili hatufanyi kampeni hata kidogo, huu ni mwendelezo wa maandalizi ya chaguzi mbalimbali. Kama mnakumbuka tulianza kujiandaa na uchaguzi wa mwaka 2015 baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010,” alisema Mbowe na kuongeza;
“Kwa sasa tunachokifanya ni kuongeza nguvu na umakini zaidi. Makundi yataanzia katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Ruvuma, tutapita kila Kata ambazo utafanyika uchaguzi wa madiwani.”
Mbowe alisema operesheni hiyo itapiga kambi katika Jimbo la Kalenga ambalo kwa sasa lipo wazi baada ya mbunge wake ambaye pia alikuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa kufariki dunia Januari 1, mwaka huu nchini Afrika Kusini.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) haijatangaza kufanyika uchaguzi katika jimbo hilo, Chadema tutafika Kalenga na tutafanya mkutano maalumu na kutoa pole kwa wakazi wa jimbo hilo kutokana na msiba mkubwa wa mbunge wao,” alisema Mbowe.
Operesheni hiyo inafanyika siku chache tangu chama hicho kikuu cha upinzani nchini kipite katika mgogoro ambao ulisababisha aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe kukimbilia mahakamani ili kunusuru uanachama wake.
Wakati Zitto akinusurika kufukuzwa kutokana na zuio la mahakama, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo walifukuzwa uanachama, likiwa ni hitimisho la mchakato ulioanza kwa kuwavua nyadhifa zao pamoja na Zitto.
Daftari la wapigakura
Mbowe alisema msimamo wa chama chake ni kutaka daftari la kudumu la wapigakura lifanyiwe marekebisho kabla ya kupigwa kwa kura za maoni kwa ajili ya kupitisha Katiba Mpya.
“Tutagomea upigaji wa kura na tutawahamasisha wananchi kugomea kupiga kura. Serikali ya CCM isijidanganye kwa kuweka mikakati ya kukwamisha zoezi hili,” alisema Mbowe.
Alisema kama Serikali inataka amani iendelee kuwepo isifanye mzaha katika mchakato wa Katiba Mpya kwa maelezo kuwa Katiba siyo mali ya vyama vya siasa, bali ni mali ya wananchi.
“Katiba siyo ya  Chadema, CUF wala NCCR-Mageuzi. Sheria inaeleza wazi kwamba daftari la wapigakura ni lazima lifanyiwe marekebisho mara mbili baada ya Uchaguzi Mkuu na kabla ya kuanza Uchaguzi Mkuu mwingine lakini hilo halijafanyika mpaka sasa licha ya Uchaguzi Mkuu  kufanyika miaka minne iliyopita,” alisema Mbowe.
Alisema wapo Watanzania waliohama maeneo yao ya awali, waliopoteza vitambulisho, waliofikisha umri wa kupiga kura na kusisitiza kuwa kuwaacha watu hao nje ya mfumo wa kupiga kura ni kuwanyima haki yao ya Kikatiba.
“Kwa mujibu wa utafiti tulioufanya tumebaini kuwa wapo watu zaidi ya milioni 5 wanaohitaji kuingizwa katika daftari la wapigakura,” alisema Mbowe na kuongeza;
“Kama Katiba haitapita kwa sababu ya kutokuboreshwa kwa daftari la wapigakura hatutarudi katika Katiba ya sasa hiyo ni ndoto.”

Ushabiki unavyowatesa vijana katika siasa

Dar es Salaam. Mwamko wa vijana katika siasa ulianza kujitokeza katika kipindi cha uchaguzi wa mwaka 1995. Chama Cha Mapinduzi (CCM) mbali na mwamko wa vijana ulioibuka ndani yake, pia kilianza kupata upinzani mkali na kutupiwa lawama na kila aina ya kejeli kwa madai ya viongozi wake kukosa sifa za kuongoza nchi.
Mwamko huo kwa vijana umeendelea kukua kwa kasi mpaka sasa kupitia uhamasishaji wa makundi mbalimbali ya wanaharakati, wasomi na huo ukawa ni mwanzo wa baadhi ya vyama vya siasa kuona umuhimu wao, hivyo kila chama kuwavuta upande ke kwa maslahi yake.
Idadi kubwa kati ya vijana hao ni wahitimu wa vyuo mbalimbali na walioko vyuo vikuu ambao ni rahisi kupokea agenda za vyama husika na kuziendeleza, hivyo kutimiza malengo ya vyama husika.
Pamoja na hao, wapo vijana wenye elimu ya wastani, na wengine walioikosa kabisa, ambao ni rahisi kufanya lolote bila kujali matokeo yake, kwa kuwa wao ni ‘bendera fuata upepo’.
Kwa hali ya siasa ilivyo nchini, baadhi ya vijana wameanza kujikuta njiapanda, wakishindwa kuchagua ni chama gani, mwanasiasa yupi au kundi lipi linaweza kuwa tumaini jipya kwao.
Hatua hiyo inatokana na udhaifu unaoendelea kuonekana ndani ya vyama vya siasa, hususani vile vyenye ushindani mkubwa katika kipindi fulani – kama ilivyokuwa kwa NCCR na CCM mwaka 1995; CCM vs CUF mwaka 2000; na CCM vs Chadema mwaka 2010 na sasa tunapoelekea 2015.
Sote ni mashuhuda wa mivutano iliyopo, vurugu na tuhuma mbalimbali za mara kwa mara zisizokuwa na majibu.
Vuguvu hilo la vijana limeanza kuingia hata ndani ya vyama vyewenye, mfano ni katika uchaguzi wa Umoja wa Vijana wa CCM mwaka juzi, na hivi karibuni katika sakata la Chadema dhidi ya Zitto Kabwe.
Katika matukio hayo, tumeshuhudia jinsi vijana walivyoamua kupigana wao kwa wao, kila upande ukitaka kutimiza malengo yake.
Kutokana na mazingira hayo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wanaeleza mitazamo mbalimbali inayosababisha vijana kuathiriwa na mapenzi ya vyama, au watu binafsi ndani ya vyama hivyo mpaka kufikia hatua ya kukosa uvumilivu, wakiamini kuwa chama hicho au watu hao ndio suluhisho la matatizo yao.
Vijana wanapotoka?
Tofauti na fikra za vijana hao, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Slaam (UDSM), Bashiru Ali anasema mpaka sasa haamini kama kuna chama chochote cha siasa duniani kilichowahi kuwa na historia ya kuleta mabadiliko ya kuikomboa jamii kuondokana na changamoto zinazoikabili.
Bashiru anasema kila chama kimekuwa na ajenda ya kuhakikisha kinashika dola pasipo kuangalia au kupigania mabadiliko katika huduma za kijamii.
“Vyama huwa na ajenda ambazo vinaona zitafaa kuwatengenezea mazingira ya kufanikisha itikadi zao. Mfano kodi za nyumba zimekuwa zikiongezeka kila wakati na hatujasikia chama hata kimoja kimesimama kulisemea, ni changamoto inayowagusa wananchi na maisha yao, kwani wanasiasa hawaoni?”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya kiraia inayofuatilia mwenendo wa Bunge nchini (CPW), Marcossy Albanie anasema hatua ya vijana kupigana inatokana na hali tofauti na matumaini waliyokuwa nayo ndani ya chama.
“Wamewekeza kwa muda mrefu wakiamini ndiyo sehemu ya kuleta mapinduzi mapya  ya kiutawala, sasa inapotokea mivutano kama tukio la Chadema, matokea yake wanakosa uvumilivu,” anasema na kuongeza;
Kina nani hawajitambui?
Katibu wa Hamasa na Chpikizi katika Umoja wa Vijana wa VCCM, Paul Makonda anasema bila kuangalia itikadi za vyama vya siasa, tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mpaka sasa asilimia 75 ya vijana hawajatambua itikadi za kisiasa.
Anasema mbaya zaidi miongoni wasiojitambua ni wasomi wengi waliohitimu elimu za vyuo vikuu.
“Hawajui siasa, hawajui itikadi ni nini na hawajui hata wanachokitaka kupitia vyama vya siasa, ila picha iliyopo kwa sasa wamekuwa wakifuata ushabiki tu wa kisiasa na kuangalia mwanasiasa gani, kundi au chama gani kinachozungumzia hisia zao,” anasema Makonda.
Kiongozi huyo aongeza kuwa kundi jingine la vijana sawa na asilimia 25 ni lenye ujasiri lakini linaishi kwa hofu na woga, linakosa nguvu ya kuhoji udhaifu uliopo katika mfumo wa vyama kutokana na nguvu za wanasiasa wachache wanaotaka kulinda maslahi yao.
Anasema kutokana na mazingira hayo, mwasiasa amekuwa akitumia fimbo hiyo kama udhaifu wa kuendelea kumtumia kijana katika jambo lolote analohitaji kupenyeza maslahi yake kwa wakati fulani.
Makonda anasema mbaya zaidi mpaka sasa taifa halina mfumo wa kuwaandaa vijana katika uelewa wa itikadi za kisiasa ndani ya vyama.
“Kutokana na hali hiyo ukijumlisha na uvivu wa kufikiri hoja na maazimio ya wanasiasa, matokeo yake vijana wanapigana ovyo wao kwa wao au kuwa watumwa wa wanasiasa,” anasema Makonda.
Nini Kifanyike?
Bashiru anasema hatua ya kwanza katika kuwakomboa vijana hapa nchini ni pomoja na kuwasaidia waweze kufikiri na kuchambua kwa makini kila hoja inayotolewa na mwanasiasa yeyote.
Anasema uwezo wa vijana ujengeke mpaka kufikia hatua ya kutengeneza msimamo na ajenda zao kama vijana.
“Tunataka tuone vyama vya siasa ndiyo vinafuata ajenda za vijana, siyo vijana wanafuata ajenda za wanasiasa, matokeo yake wanajikuta kwenye mpasuko wa makundi,” anasema.
Bashiru anasema uelewa mdogo wa vijana katika kuchambua itikadi za kisiasa hapa nchini utaendelea kuwa changamoto mpaka pale vijana wanakapokuwa tayari kufanya mabadiliko.
“Vijana watengeneze vyama vyao kwa ajili ya kupigania maslahi yao, waunde vyama ambavyo vitakuwa na ajenda ambazo zitakuwa na ushawishi wa kutumiwa hata na hao wanasiasa, kama ambavyo tuliwahi kuwa na vyama vya wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara,” anasema Bashiru.

Chuki zaanza ndani ya CCM, Sinyanga, Monduli, Mgeja, Lowasa

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja ameonya baadhi ya viongozi wa chama hicho kuwajengea chuki wanachama kadhaa na viongozi kwa madai wako karibu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.
Hatua ya Mgeja imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Geita, Joseph Kasheku ‘Msukuma’ kumkana na kumshutumu, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai kuwa anawalazimisha kuwa nyuma ya Lowassa wakati sivyo ilivyo.
Hata hivyo, Msindai alikanusha madai hayo kuwa hakuwahi kuwazungumzia wenyeviti wa CCM wa mikoa kuwa nyuma ya Lowassa zaidi ya kusema kuwa wanamuunga mkono katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu, Mgeja alimtetea Msindai kuhusu suala la wenyeviti wa CCM kuwa nyuma ya Lowassa katika urais. Alisema: “Nataka kutoa angalizo kwa viongozi ndani ya chama, Tanzania kwa ujumla, kumejitokeza tabia ya baadhi ya watu kuchukiana eti tu kwa sababu wako nyuma ya Lowassa,” alisema na kuongeza:
“Kumeanza watu kuchukiana, kuhukumiana kwa sababu uko karibu na Lowassa au kuwa na imani naye katika utendaji kazi wake, kumpenda na kumkubali mtu ni utashi wa mtu binafsi...tusihukumiane wala kuchaguliana marafiki,” alisema Mgeja.
Mgeja alisema: “Hakuna dhambi ya kumpenda au kumwamini Lowassa, lakini watu wanachukia, watu wananung’unika, wananuna haya yote ni majungu, woga, wivu na kutokujiamini. Inawezekana wanaofanya hivyo, wanatumwa na walio nyuma yao.
“Katika kipindi cha kuelekea uchaguzi, tusianze kusakana uchawi, muda ukifika, kila mtu atabebwa kwa sifa zake na atajibeba kwa umahiri wake.”
Mgeja alisema, kazi kubwa inayotakiwa kufanyika kwa wabunge, mawaziri na viongozi wa kada mbalimbali ni kukaa chini na kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha wanapata maji safi, dawa hospitalini na elimu kuliko kutumia muda mwingi kuangalia nani anampenda Lowassa.
“Kuna changamoto nyingi zinazowakabili wananchi na kila siku wanatuangalia viongozi, suala la vijana ni tatizo kubwa huduma za msingi kuliko kukaa na kuangalia Lowassa anafanya nini na yuko na nani, haileti tija hata kidogo,” alisema.
Mgeja aliwataka wanaCCM kutulia na kutafakari mambo ya maendeleo kwa kuwa hakuna mtu aliyejitangaza urais akiwamo Lowassa zaidi ya kuanzisha safari ya matumaini ambayo ndani yake kuna mafanikio katika elimu, huduma za afya, ajira kwa vijana na mambo mengi,” alisema.
Hivi karibuni, Msindai alikaririwa akisema: “Mimi ni Mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM, lakini sikuwahi kuzungumza kuwa wenyeviti wote wanamwunga mkono Lowassa katika Uchaguzi Mkuu 2015... kikubwa tulichozungumza ni kumuunga mkono katika safari yake ya mafanikio katika kuendeleza elimu, maji, ujenzi wa zahanati.”
Msindai alisema wanamwangalia Lowassa kutokana na uwezo wake katika kusimamia mipango yake ya maendeleo na zaidi katika kupigania elimu pana kwa Watanzania.

Ana umri wa miaka 12, aolewa kwa ng’ombe 15

Kiteto. Wamasai ni miongoni wa jamii chache duniani, ambazo zimefanikiwa hadi sasa kudumisha mila zake. Katika mila za jamii hii, zipo ambazo zinapaswa kuendelezwa na nyingine zinapaswa kupigwa marufuku.
Miongoni mwa mila ambazo zinapaswa kuendelezwa ni pamoja na kuendelea kutambua na kuheshimu viongozi wa mila ‘Laigwanaji’ kuheshimu viongozi wa rika na Serikali, kuishi kwa umoja na kudumisha tamaduni.
Mila ambazo zimepitwa na wakati katika jamii hii ni pamoja na kurithi wajane, ukeketaji watoto na kuoa watoto wadogo.
Katika makala hii, leo nitazungumzia mila ya kuoa watoto wadogo kama nilivyobaini katika vijiji kadhaa wanapoishi Wamasai, wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara.
Nikiwa katika uchunguzi wa mapigano baina ya wafugaji wa Kimasai na wakulima katika vijiji saba vinavyozunguka eneo la Hifadhi ya Emborey Murtangosi nakutana na mtoto wa miaka 12 aliyeolewa.
Nilipata bahati ya kufika katika familia ya mtoto huyu, katika Kitongoji cha Ndiligishi kaya ya Engusero Sidani baada ya kuwa ni moja ya familia ambazo zimeathirika na mapigano baada ya kuchomewa makazi na kuibiwa vyakula.
Wakati nahojiana na wanafamilia napata fursa ya kuonana na mtoto huyo aliyegeuzwa kuwa mke, nashawishika kumuhoji baada ya kuona akiwa amejitenga na watoto wenzake huku akiwa na mawazo.
Mtoto huyo ambaye jina lake tumelihifadhi kutokana na sababu za kimaadili, hajui kiswahili  vizuri, hivyo nalazimika kumuomba mtoto mwenzake, Stela Paulo aje anisaidie kuongea naye.
Ananieleza kuwa yeye ni mke wa Lembau Leseri  na ameolewa  mke wa pili na ana miaka miwili ya ndoa.
Akiwa  anaonekana kutokuwa na raha ya maisha, mtoto huyo anasema wazazi wake, ndio walimpeleka kwa mwanaume baada ya kupewa mahali.
Anasema hajui kusoma wala kuandika kwani hakufanikiwa kupelekwa shule na wazazi wake.
Ninapomdadisi kama angependa kusoma, anasema angepata fursa hiyo angefurahi lakini sasa haiwezekani tena kwani ni mke mtu.
Kwa umri wake na umbile bado ni mdogo lakini, anaeleza huku akiwa kichwa chini na kwa aibu kuwa majukumu yote muhimu kwa mume wake aliyepewa na wazazi anafanya.
Hata hivyo, mtoto huyu anaonekana afya yake kudhoofika kutokana na maradhi ya ngozi na huenda na majukumu ya kifamilia.
Mume wa mtoto azungumza.
Mume wa mtoto huyo, Lembau Leseri hivi sasa ni mgonjwa na takriban wiki mbili, alikuwa amelazwa hospitali ya kiteto kutokana na kutokewa na majipu mwilini.
Ananieleza kuwa, mtoto huyo ni mke wake wa pili, ambaye alimuoa kutoka kijiji jirani cha Taiko.
Anasema mke wake wa kwanza, Kawie Lembau sasa ana watoto saba.
Lembau haoni kama amefanya makosa kuoa mtoto mdogo, kwani ananieleza kuwa alimuoa kwa ng’ombe 15.
Hata hivyo, anaeleza maisha yake ya ndoa na mtoto huyo, hayakuwa ya taabu kwa mwaka mmoja uliopita lakini sasa ana matatizo kutokana na kukabiliwa na maradhi.
“Sijui naumwa nini kwani nimelazwa hospitali na wamenipa dawa nirudi nyumbani,” anasema.
Anasema licha ya maradhi yanayomkabili,  maisha yamekuwa ya magumu, mapigano ya ardhi yameifanya familia yake kukosa chakula kwani zaidi ya magunia 50 ya mahindi yaliibwa.
Anasema pia vijana wa kiume wa familia yao, wamekimbia kwa sababu  polisi wanaendesha msako kuwakamata waliohusika na mauwaji ya wakulima tisa kutokana na mapigano ya ardhi.
“Hali ni ngumu, mimi naumwa siwezi kutembelea umbali mrefu kutafuta chakula, vijana wa hapa wamekimbia wanaogopa polisi,”anasema Lembau
Hali ya njaa katika familia hiyo yenye maboma matatu, inathibitishwa na jinsi nilivyoikuta akina mama wazee na watoto wadogo walikuwa wakichemsha mchicha majira ya saa saba lakini hadi naondoka takriban saa tisa walikuwa hawajala chakula kingine.
Mke mkubwa
Mke mwingine wa Lembau ambaye anaonekana ni mtu mzima ni mkimya na nilipotaka anieleze kuhusiana na mke mwenza wake  anashindwa kusema kitu na anaingia ndani ya boma lao.
Lakini natambua kwa mila za kimasai ni nadra sana mwanamke kuwa na ujasiri kupingana na mwanaume kutokana na misingi ya mila na desturi zao.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wazungumza.
Shilinde Ngalula ni Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), anapatwa na mshangao anapoelezwa mtoto huyo ni mke wa mtu hasa kutokana na umri wake mdogo.
Hata hivyo, baada ya kuzungumza naye anaeleza kusikitishwa na maisha ya ndoa ya mtoto huyu.
“Hili ni tatizo kubwa katika jamii hizi kwani mtoto huyu alipaswa kuwa shule lakini kaolewa na mtu mzima ambaye sasa ni mgonjwa,”anasema Shillinde.
Shilinde na maafisa wengine wa LHRC ambao wanafanya uchunguzi wa mapigano baina ya wakulima na wafugaji wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara, anaahidi kutafuta muda muafaka kufuatilia maisha ya mtoto huyo.
“Jamii hizi za pembezoni zinakabiliwa na matatizo mengi ambayo mengine yanatokana na kutokuwa na mazingira bora ya kupata elimu na huduma nyingine muhimu”
Shillinde hata hivyo, anaongeza kuwa umefika wakati, Serikali na wadau wengine kufika maeneo ya vijiji katika jamii kama za kimasai ili kusaidia kutatua matatizo yao ikiwepo ya umasikini,elimu na mila zilizopitwa na wakati.
Je, maisha ya ndoa ya mtoto huyu yataendelea vipi kwa sasa kwani licha ya kuwa na umri mdogo bado ana mzigo mkubwa wa kumuuguza mume wake na je, nani atamuokoa na ndoa ya utotoni na kumrejesha shule kwa watoto wenzake?
Hili ni swali zito lisilo na jibu kwa sasa hata hivyo huenda LHRC wakalivalia njuga suala hilo na haki kupatikana kama ambavyo tayari wameahidi.

Kikwete afunga mjadala wa gesi

Dar es Salaam: Rais Jakaya Kikwete amefunga mjadala wa wafanyabiashara wazawa wanaotaka kupewa kipaumbele katika uwekezaji wa sekta ya gesi akisema Shirika la Maendeleo la Petroli(TPDC) linajitosheleza kuwasaidia Watanzania wanufaike na rasilimali hiyo.
Katika kipindi cha miaka miwili, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameshikilia kuwa hakuna Watanzania wenye uwezo wa utafutaji, uchimbaji na uzalishaji, jambo ambalo linapingwa vikali na wafanyabiashara wazawa.
Akizungumza jana wakati wa Kongamano la Viongozi wa Dini kuhusu rasilimali ya gesi, mafuta na madini kwa ajili ya amani na maendeleo ya taifa, Rais Jakaya Kikwete alisema hakuna kampuni nchini yenye dhamana ya kupata mikopo kwa ajili ya kuwekeza katika sekta hiyo.
“Kampuni za kigeni zenye mitaji mikubwa zinafanikiwa kupata mikopo kwa kuwa zina dhamana inayowasaidia kupata mikopo kwenye mabenki,” alisema.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema kama kuna kampuni za Watanzania zinatakiwa kushirikiana na wawekezaji watapaswa kufuata taratibu zilizowekwa.
Rais Kikwete alisema uwekezaji kwenye sekta ya mafuta ni kama mchezo wa kamari kwani mtu anaweza kuwekeza fedha nyingi katika utafutaji wa gesi na asipate kitu.
“Ni kampuni gani Tanzania ambayo itakuwa tayari kucheza kamari?” alihoji Rais Kikwete.
Alisema ndio maana Serikali imeona ni vizuri iandae mpango wa kuiwezesha TPDC kuingia kwenye shughuli za gesi badala ya kuwa kutoa leseni tu.
“Tunataka siku moja TPDC iwe na uwezo wa kuwauzia hisa Watanzania iwe kama kampuni kubwa za Statoil(Norway) na Petro Plus(Brazil) zinazoendeshwa na Serikali zao,” alisema.
Rais Kikwete alisema baada ya kuliwezesha shirika hilo, Watanzania watanufaika kwa kiwango kikubwa tofauti na kutoa kipaumbele kwa kampuni binafsi za Watanzania.
Washiriki watoa maoni tofauti
Mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk Charles Kitima alipinga kongamano hilo kufanyika sasa kwani alieleza lilipaswa kufanyika miaka mitano iliyopita na sio sasa wakati ambapo shughuli za uchimbaji wa gesi zinakaribia kuanza.
Akizungumza wakati wa akisoma salamu za viongozi wa Dini ya Kikristo katika kongamano hilo, Dk Kitima alisema kongamano kama hilo haliwezi kubadili chochote na kinachofanyika ni kwa wawekezaji kujifagilia njia wakati wanaelekea katika kuanza kutekeleza miradi waliyowekeza.
“Hapa ninachoweza kusema ni kuwa wafadhili hao wametoa fedha, wamefadhili kongamano hili ili wakianza shughuli zao wasisumbuliwe,” alisema na kuongeza kuwa kinachofanyika sasa hakitoi taswira nzuri kwani jamii imelishwa sumu kuwa haiwezi kufanya lolote bila kuombaomba.
Akionekana kujibu hoja hiyo, Askofu Stephen Munga wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), aliomba kuweka sawa dhana hiyo kwa kusema kuwa sio sahihi kuwa mkutano huo umefadhiliwa na matajiri wa gesi na mafuta.
“Kongamano tumeandaa wenyewe baada ya baadhi ya maaskofu wa KKKT kufika ofisini kwa Waziri wa Nishati na Madini, Muhongo kuzungumza nae kuhusiana na uharibifu wa mazingira na akataka pia tuzungumzie suala la gesi, ndio tukaona kuna haja ya kufanya kitu kama hiki ambacho kinafanyika sasa,” alisema.
Naye Sheikh Aboubakary Zuberi alisema ni vizuri watu ambao wanaishi katika maeneo ambako rasilimali zinapatikana ni vizuri wakanufaika nazo badala ya kuwa kama ilivyo sasa jambo ambalo haliwezi kuleta matokeo mazuri siku za mbeleni.
Alisema nchini kuna mgawanyiko mkubwa wa mapato jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi.

Tuesday, 21 January 2014

Mbatia ashinda tena NCCR, mizengwe yatawala mkutano

Dar es Salaam. Uchaguzi Mkuu wa nane wa Chama cha NCCR-Mageuzi, umemchagua tena James Mbatia kuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa kipindi kingine cha miaka mitano ijayo huku mizengwe ikitawala katika uchaguzi huo.
Katika uchaguzi huo ulioanza juzi, idadi kubwa ya wajumbe walikuwa na mkakati wa kumng’oa Katibu Mkuu, Samwel Ruhuza aliyekuwa akitetea nafasi yake, Mosena Nyambabe na Rehema Sam waliokuwa wakiitaka nafasi hiyo.
Wajumbe walikuwa na mpango huo kwa kuwa Nyambabe yuko vizuri kiutendaji ikilinganisha Ruhuza. Jana kwa nyakati tofauti, wajumbe walionekana katika makundi kujadili hali hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Mbatia.
Ukiacha hali hiyo, Mbatia alipata upinzani mkali akichuana kwa mbali na aliyekuwa Kamishna wa chama hicho Mkoa wa Katavi, Charles Makofila, ambaye ni mlemavu wa viungo.
Tangu kuanza kwa mkutano huo katika Ukumbi wa Diomond Jubileee, hapakuwa na dalili za upinzani wa nafasi hiyo ya uenyekiti na baadhi wa wajumbe wa mkutano walisikika wakisema, “Makofila bwana sijui amekosa cha kufanya, ila ndo hivyo wacha amsindikize mwenzake.”
Zoezi la upigaji kura lilianza saa 10 jioni hadi saa moja usiku chini ya Msimamizi wa Uchaguzi huo, Moses Machalli.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe 228 kati ya 289.
Machalli akitangaza matokeo hayo alisema, Mbatia ameshinda kwa kura 201 na Makofila ameambulia kura 26 na kura moja imeharibika.
“Ndugu Mbatia atakiongoza chama hiki kuanza hii leo (jana) hadi Januari 2019 hivyo tumuunge mkono na uchaguzi usiwe chanzo cha migogoro, tumemaliza salama na sasa tunaangalia mbele,” alisema Machalli.
Mbatia akitoa shukrani zake alisema, “Nawashukuru sana kwa kutumia demokrasia yenu kunichagua, nawaahidi kuwatumikia kwa moyo wangu wote, uchaguzi umekwisha sasa tujenge chama chetu.”
Mwenyekiti huyo mpya, aliwataka wabunge wa chama hicho kuacha kubweteka katika majimbo yao na sasa wazunguke nchi nzima kukijenga chama.
“Machali, Kafulila kumbukeni kulipa fadhila za chama, zungukeni nchi nzima acheni kujisahau bila NCCR tusingekuwa katika Bunge tukufu, sasa kazi kwenu kwani tunaweza kama tutaamua,” alisema Mbatia.
Akiongea baada ya kutangazwa matokeo, Makofila alisema uchaguzi ulifanyika kwa uhuru na uwazi ila wajumbe wa mkutano huo waliomnyima kura wamepoteza kura zao.
“Niliwaahidi ningeongeza posho za mkutano kutoka elfu 30 hadi elfu 60 sasa kwa kuwa hawakunichagua wamepoteza kura zao,” alisema Makofila.
Makofila alisema kushindwa kwake hakutamfanya ajitoe ndani ya NCCR ila atatumia kipindi hiki kuongeza elimu ambayo hadi kufika uchaguzi mwingine mapema mwaka 2019 atakuwa amejiimarisha zaidi.
Katika uchaguzi huo ambao haukuwa na ushindani katika nafasi nyingi kutokana na baadhi ya nafasi kujitokeza wagombea wanaokidhi nafasi husika hivyo kuwachagua kwa kura za ndiyo au hapana.
Mfano ni nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Tanzania Bara na Visiwani hapakuwa na washindani hivyo wajumbe walipiga kura za ndiyo na hapana.

Ndoa ya Obama, Michelle shakani

Marekani. Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa vyanzo vya ndani vya Ikulu ya Marekani, wenza hao wamekuwa katika migogoro na Obama alilazimika kusherehekea sherehe za mwaka mpya mjini Hawaii akiwa na binti zake wawili, Sasha na Malia bila kuwepo Michelle.
Jarida la National Enquirer lilieleza kwamba katika moja ya matukio, Obama aliwahi kukutwa akiwa na mwanamke mwingine katika ‘mazingira ya kutatanisha’ wakati mkewe akiwa safarini.
Kutokana na ripoti iliyotolewa na Bombshel , Michelle na Obama wamekuwa wakilala vyumba tofauti ndani ya Ikulu. Michelle pia anajiandaa kuhama katika jumba lao pale Chicago ambalo wameishi wakati wa uchumba wao miaka 21 iliyopita na kwa msisitizo watajadili juu ya talaka.
Taarifa ilidai tatizo limeanza miaka minane iliyopita pale Obama alipodhamiria kujijenga kisasa. Ni mtoto wao Sasha ambaye aliumwa ugonjwa unaosababishwa na woga wa maisha unaoitwa Spinal Meningitis ndiyo uliowafanya waendelee kuwa pamoja.
Kitabu cha Anderson kinaelezea tatizo lilivyoanza baada ya Barack Obama kuamua kuingia kwenye siasa, ambapo Michelle alisikika akimwambia mumewe; “Wewe unajifikiria mwenyewe tu.”
Naye Barack Obama amesikika akisema: “Sikuwahi kufikiri kamwe kwamba ningelea familia mwenyewe siku moja.” Anderson anadai kuwa Obama amechoshwa na malalamishi ya mkewe.
“Nampenda sana Michelle lakini ananiumiza na ubishi wake wa kila mara,” alisikika akisema Obama na kuongeza kuwa; “Anaonekana ni mwingi wa machungu na hasira siku zote.”
Akizungumza na televisheni ya CBS ya Marekani, Anderson alidai kuwa ilikuwa nusura Michelle atembee nje ya ndoa kwa sababu ya upweke.
Kwa miaka mitano wamekuwa na wasiwasi juu ya uwezo wao wa kupata watoto kabla Malia hajazaliwa. Walishajadili sana suala la kuasilia watoto (adoption) na marafiki zake wa karibu lakini kwa bahati nzuri Malia alizaliwa mwaka 1998 na kuondoa wazo hilo.
Jina kamili la Obama ni Barack “Barry” Hussein Obama, Jr, alizaliwa Agosti 4, 1961 Honolulu, Hawaii, alikulia huko huko Hawaii na Indonesia, baba yake mzazi ana asili ya Kenya. Jina kamili la mkewe ni Michelle LaVaughn Robinson, alizaliwa Januari 17, 1964 Chicago, Illinois.
Kukutana kwako
Barack na Michelle walikutana mwaka 1989 katika mazingira ya kikazi, walifunga ndoa Oktoba 18, 1992, katika Kanisa la Umoja wa Kristu la Trinity lililopo Chicago, Illinois.
Lakini vyanzo vingine vya taarifa zinadai kuwa ndoa haiko imara, hasa baada ya tukio la Obama kupiga picha za pamoja bila aibu na Waziri Mkuu wa Denmark, Helle Thorning-Schmidt (46) wakati wa mazishi ya aliyekuwa rais wa kwanza wa Afrka Kusini, Neslon Madiba Mandela.
Obama akiwa na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, alikuwa akicheka na kumnong’oneza kitu waziri huyo mara kwa mara kwa muda wote, huku Michelle akiwa pembeni yake amenuna. Mara nyingi alikuwa akimshika shika mabega.
“Lakini kwa sasa Michelle anajiona kanyanyasika na kuaibishwa mbele ya dunia kwani picha hizo zilirushwa duniani kote kupitia televisheni, magazeti na mitandao mbalimbali. Alisikika akimtapikia Obama huku akisema “Nimechoshwa.”
Pia tatizo limekuzwa na safari ya kikazi ya Obama hivi karibuni kule Thailand ambayo ilimkutanisha na Waziri Mkuu mrembo kuliko pengine wote duniani , Yingluck Shinawatra.
Tarifa zaidi zilieleza kwamba usalama wa taifa nchini humo unafahamu kuhusu suala hilo, lakini umekuwa ukilichukulia kama suala binafsi na Michelle alionekana kukasirishwa kupita kiasi alipopata taarifa hizo.
“Baada ya tukio hilo Michelle aliamua kuwasiliana na mwanasheria wake akitaka kujua namna ya kuomba talaka na alimwambia Obama kwamba anahitaji kuishi mbali naye,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa makubaliano waliyofikia, ilielezwa kwamba Michelle ataendelea kuishi mjini Washington DC hadi binti yao mdogo, Sasha (12) atakapomaliza elimu yake ya sekondari. Binti yao mkubwa, Malia (15) tayari ameshaingia sekondari.
“Michelle (50) kwa sasa ataendelea kuishi kwenye Ikulu ya Washington hadi Obama atakapomaliza muda wake wa urais ili tu aweze kuonekana kama yupo, lakini aliweka wazi kabisa kwamba wataishi maisha tofauti,” ilieleza ripoti hiyo ikimkariri mmoja wa vyanzo kutoka Ikulu hiyo. Ripoti hiyo ilikariri chanzo hicho kikieleza; “Michelle kwa sasa anaishi katika vyumba vya watumishi kwenye nyumba yao ya familia na anajiandaa kuchukua vifaa vyake na kuvipeleka kwenye nyumba yao binafsi ya Chicago”.
Taarifa nyingine ilieleza kwamba tayari mambo baina ya wanandoa hao yameshakuwa magumu kiasi kwamba wamekuwa wakiishi kwenye vyumba tofauti katika Ikulu ya Marekani.
Mgogoro wao
Barack na Michelle wamekuwa katika mgogoro kwa miaka kadhaa na wanalazimika kuwepo pamoja kwa sababu tu ya watoto wao na kulinda hadhi yake kisiasa. Lakini kwa sasa Michelle amekuwa mkali kweli kweli. Anaona kama amepuuzwa na kudhalilishwa mbele ya dunia nzima na amekuwa akipiga kelele akisema, “Nimevumilia vya kutosha”, taarifa zaidi zilieleza.
Kwa sasa Michelle anaonekana kupigania kukamilisha namna ya kupata talaka, lakini baadhi ya taarifa zinaeleza kwamba anafanya makusudi kuuchelewesha ili aweze kuukamilisha baada tu ya Obama kumalizia muda wake wa urais ambapo ataweza kupata Dola za Marekani 30 milioni kupitia mpango wa vitabu na zaidi ya dola 65 milioni kwa kuonekana hadharani.
“Kwa sasa Barack anaonekana kama amemwaibisha Michelle mbele ya dunia na kwa hili ni wazi kwamba atalilipa kwa gharama kubwa,” kilieleza chanzo kutoka Ikulu ya Marekani.
“Ni jambio lililo wazi kwa sasa kwamba Michelle ameshamwambia Obama kwamba anahitaji kuishi mbali naye, japokuwa kwa sasa imekuwa ni suala gumu kwa kuwa anahitaji aendelee kuonekana wakiwa pamoja kwa sababu muhimu, lakini wanapokuwa nyumbani wanaishi maisha tofauti ya kutengana,” kilieleza chanzo hicho.
Iwapo taarifa hizo ni sahihi, hii inamaanisha kwamba Michelle ameudhika kupindukia na hii si mara ya kwanza jambo hilo kutokea miongoni mwao.
Tangu Obama alipochaguliwa kuwa rais, vitabu viwili vimemtaja vikidai kwamba wenza hao walikaribia kutengana katika kipindi cha miaka yao ya mwanzo ya ndoa na hata Michelle alifikia hatua ya kutaka kuomba talaka akidai kwamba anaona maisha yake ya kisiasa yanawanyima furaha na kuwa pamoja nyumbani.
Mwaka 2009 mwandishi wa siku nyingi wa Washington, Richard Wolffe alisema kwamba ndoa hiyo ilikuwa sawa na iliyovunjika miaka tisa kabla kutokana na harakati za kisiasa za Obama zilizokuwa zikimsababisha asiwe karibu na familia kwa muda mrefu.
“Kulikuwa na mawasiliano kidogo sana na familia yake na hata mapenzi yalipungua. Michelle alikasirishwa sana na hali hiyo akilaumu kwamba mumewe anaonekana kuwa mbinafsi; ilimpa wakati mgumu sana,” aliandika Wollfe.
Wakati huo Michelle alilazimika kutulia kwa kuwa tayari alishakuwa mama, mbinti zao awili, Malia na Sasha kwa sasa wana miaka 15 na 12. Mumewe ambaye walikutana kwa mara ya kwanza walipokuwa wakifanya kazi kwenye shirika moja la sheria mjini Chicago mwaka 1989, alikuwa ndiyo kwanza amechaguliwa kuwa Seneta wa Illinois na alikuwa akijipanga pia kuwania nafasi kwenye baraza la Congress.
Mke wa Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, Carla Bruni alipoulizwa katika moja ya vitabu kuhusu uzoefu wake wa maisha ndani ya Ikulu alijibu, ‘Acha kabisa! Usiulize ni kama jehanamu. Sikuwahi kuyafurahia’ ambapo Michelle alisema hakuwahi kuzungumza maneno ya aina hiyo.
Mwaka 2012 mmoja wa waandishi wa masuala ya siasa, Edward Klein alieleza kwamba Obama alionekana mwenye mawazo kupita kiasi, wakati ndoa yake ilipokuwa kwenye matatizo mwaka 2000 kiasi kwamba rafiki zake walihofu kwamba anaweza kujiua.
Alieleza kwamba Michelle alikuwa mwenye hasira kwa kuwa alimkataza Obama kuwania nafasi kwenye Congress, ushauri ambao hakuufuata na hata hivyo alishindwa kwenye uchaguzi.
“Baada ya kushindwa alirejea kwa Michelle kwa ajili ya kupata pumziko. Lakini Michelle hakuwa tayari kuonyesha huruma yoyote,” aliandika Klein aliyedai kwamba marafiki wa Michelle walimweleza kuwa tayari ameshafungua kesi akidai talaka.

Serikali yawabeba waliofeli kidato cha pili

Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakisubiri matokeo ya kidato cha pili mwaka 2013, imebaini kuwa Serikali imetoa agizo kwamba wanafunzi wote waliofeli mtihani huo kuendelea na masomo ya kidato cha tatu, huku wakisoma mafunzo ya kurudia mtihani wa kidato cha pili.
Licha ya matokeo hayo kutotangazwa hadi sasa, imebainika kuwa waliofaulu mtihani huo uliofanywa Oktoba 7 hadi 21 mwaka jana ni asilimia 62 tu, asilimia 31 wakitakiwa kukariri (kurudia) kidato cha pili mwaka huu, huku asilimia saba wakishindwa mtihani huo kwa mara ya pili.
Jumla ya wanafunzi 531,457 walitajwa na Wizara ya Elimu mwaka jana kuwa watafanya mtihani huo.
Uamuzi huo wa Serikali ni tofauti na ule uliotolewa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa Novemba 4, mwaka 2012, kwamba kuanzia wakati huo mtihani wa kidato cha pili utakuwa ni wa mchujo na kwamba atakayefeli atatimuliwa.
Dk Kawambwa alisema matokeo ya mtihani wa kidato cha pili yatatumika kama kigezo cha kuchuja na kukariri kidato cha pili kwa watahiniwa watakaoshindwa kufikia wastani wa ufaulu wa alama 30.
Alisema mtahiniwa ataruhusiwa kukariri kidato cha pili mara moja tu na endapo mtahiniwa atashindwa mtihani kwa mara ya pili kwa mwaka utakaofuatia, itabidi aendelee na elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi.
Gazeti hili limeiona barua iliyoandikwa Januari 16 mwaka huu na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kusainiwa na Katibu Mkuu wake, Profesa Sifuni Mchome, kwenda kwa wadau wa elimu nchini, wakiwamo maofisa elimu wa mikoa na Chama cha Wamiliki wa Vyuo na Shule Binafsi (Tamongsco).
Katika barua hiyo, wizara hiyo imewataka wadau hao kuhakikisha kuwa wanafunzi watakaofeli mtihani huo, wanaendelea na masomo ya kidato cha tatu.
“Matokeo ya kidato cha pili yamepokewa na kufanyiwa uchambuzi ili kupata taswira ya taifa. Taarifa ya matokeo hayo imebaini kuwa watahiniwa waliofanya mtihani na kufaulu ni sawa na asilimia 62 tu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo na kuongeza;
“Hali hii inaonyesha kuwa asilimia 31 ya wanafunzi watatakiwa kukariri kidato cha pili, 2014. Wale walioshindwa kwa mara ya pili ambao ni asilimia saba wanatakiwa kuendelea na masomo nje ya mfumo rasmi.”
Barua hiyo inaeleza kuwa wanafunzi waliofaulu kwa wastani wa alama 20 na kuendelea waendelee na masomo ya kidato cha tatu mwaka 2014, wakati awali Serikali ilitoa tamko kuwa watakaoshindwa kufikisha alama 30 watatimuliwa.
“Wanafunzi waliofaulu kwa wastani wa alama 20 hadi 39 wapewe mafunzo rekebishi ‘Remedial class’ wakiwa kidato cha tatu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Inaeleza kuwa uamuzi huo unawahusu wote wakiwamo wale walioshindwa kwa mara ya pili, “Kwa maana hiyo hakuna mwanafunzi atakayerudishwa nyumbani.”
Mwisho barua hiyo imewataka wadau hao kuhakikisha kuwa inawapa taarifa mameneja na wamiliki wa shule na seminari ili kusimamia utekelezaji wa uamuzi kuhusu matokeo hayo.
Kauli ya wizara
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Profesa Mchome alisema, “Suala la wizara kuagiza wanafunzi wote waliofeli kuendelea na masomo ya kidato cha tatu mimi sijalisikia, ninachojua ni kwamba wapo watakaorudia.”
Alisema kuwa tayari wizara imeshapeleka taarifa za matokeo hayo na uamuzi wa Serikali katika kila kanda nchini. “Kila shule ina taarifa hizo. Wapo wanafunzi watakaorudia.”
Akizungumza kuhusu matokeo ya kidato cha pili mwaka 2013 kutotoka mpaka sasa alisema, “Ninachofahamu ni kwamba matokeo ya kidato cha pili yameshawasilishwa katika kanda zote nchini.”
“Unajua matokeo ya kidato cha pili siyo kama matokeo ya darasa la saba, kidato cha nne na sita. Matokeo ya kidato cha pili ni kama mwendelezo wa tathmini ‘Continuous assessment’ kwa mwanafunzi, hutumika pia katika mtihani wa kidato cha nne.”
Alisema ndiyo maana matokeo hayo hupelekwa katika shule husika. “Baada ya kupelekwa katika shule husika, hapo ndipo inaweza kutolewa taarifa za matokeo hayo pamoja na ufafanuzi.”
Kwa nyakati tofauti gazeti hili lilimtafuta Dk Kawambwa na Naibu wake, Phillip Mulugo ili kutolea ufafanuzi suala hilo, lakini simu zao za mkononi zilikuwa zikiita bila majibu.
Msimamo wa Tamongsco
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Tamongsco, Benjamin Nkonya kueleza kama wanakubaliana na agizo hilo la Serikali alisema, “Inaonekana Serikali haiko tayari kutekeleza mkakati wake wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).”
“Kama wizara inalazimisha wanafunzi walio na ufaulu mdogo kuendelea na masomo katika mfumo wa vidato (formal education), lazima tutegemee kuona wanafunzi wakifanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne.”
Alisema kuwa asilimia 98 ya wanachama wa chama hicho ni Watanzania wazalendo kwamba hawapo tayari kutekeleza agizo la Serikali kwa sababu siyo la kizalendo na limetolewa kwa ajili ya kutimiza malengo ya kisiasa ya kujiongezea umaarufu wa muda mfupi, huku Watanzania wakiogelea kwenye dimbwi la umaskini unaotokana na ujinga.
“Wachache watakaosaliti msimamo huu watakuwa wamekubali kupoteza muda wa vijana wetu huku wakijua kwamba watafika kidato cha nne, kupata daraja sifuri na kuishia kuwa machangudoa, wauza dawa za kulevya, bangi, wizi na vitendo vingine vya uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu,” alisema.
Alisema ili kuwasaidia wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na masomo yao; “Mwanafunzi ambaye ufaulu wake utakuwa chini ya asilimia 45 aondolewe katika mfumo wa elimu ya vidato (formal education) na kuingizwa katika mfumo wa elimu ya ufundi mchundo (TVET - Technical education and vocational education).”
Alisema wanachama wa Tamongsco wanamiliki vyuo 586 kati ya vyuo 750 vya ufundi mchundo (VETA) na wanamiliki vyuo 1975 kati ya vyuo 1988 vya ufundi stadi (technical institutes) ambavyo vinasimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi Stadi (NACTE).
“Vyuo hivi vina uwezo wa kuchukua wanafunzi wote ambao wana ufaulu wa chini ya asilimia 45 kuwaendeleza hadi chuo kikuu. Kikwazo pekee kilichopo ni kwa Serikali kukubali kuchangia gharama za uendeshaji wake.”
“Kikwazo hiki kitaondoka endapo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itakubali kutekeleza sera, sheria na kanuni za ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) partnership) kama ilivyopitishwa na Bunge mwaka 2010.
Kidato cha pili 2012
Katika mtihani huo mwaka 2012 wanafunzi 136,923 kati ya 386,271 waliofanya mtihani huo walifeli. Idadi ya waliofeli ilikuwa sawa na asilimia 35.5, wakiwamo wasichana 74,020 na wavulana 62,903, waliofaulu walikuwa wanafunzi 245.9,32.

JK atema wengine watano, wapya ni 10

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri ambayo yamewatupa nje mawaziri watano, kuwaingiza 10 wapya, kuwapandisha manaibu wanne kuwa mawaziri kamili na kuwahamisha wengine wanane kutoka wizara zao kwenda nyingine.
Miongoni mwa walioachwa katika mabadiliko yaliyotangazwa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue jana, ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huvisa ambaye nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilith Mahenge.
Wengine walioachwa na wizara zao kwenye mabano ni Manaibu Waziri, Goodlucky Ole Medeye (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Gregory Teu (Viwanda na Biashara), Benedict Ole Nangoro (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) na Philipo Mulugo (Elimu na Mafunzo ya Ufundi).
Mawaziri hao wanaungana na waliokuwa mawaziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David na Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki ambao uteuzi wao ulitenguliwa na Rais kutokana na matokeo ya uchunguzi wa Kamati ya Bunge kuhusu utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Balozi Sefue alisema kuachwa kwa mawaziri hao ni moja ya hatua zilizochukuliwa na Rais Kikwete kuimarisha utendaji serikalini. Pia alisema mabadiliko hayo yametokana na kuwapo kwa nafasi baada ya kutenguliwa kwa uteuzi wa mawaziri hao na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.
“Rais amefanya mabadiliko kwa mujibu wa Ibara ya 55 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayompa mamlaka ya kutekeleza wajibu huo,” alisema Balozi Sefue.
Sura mpya
Sura 10 mpya zilizoingia katika Baraza hilo ni pamoja na Dk Asha Rose Migiro aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mbunge wa Busega, Dk Titus Kamani ambaye anakuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Naibu wake, Kaika Saning’o ole Telele ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro.
Wengine wapya ni wale walioteuliwa kuwa Naibu Mawaziri na wizara zao kwenye mabano, Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba (Fedha), Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto) na Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama (Elimu na Mafunzo ya Ufundi).
Pia wapo Mbunge wa Serengeti, Dk Steven Kwebwe (Afya na Ustawi wa Jamii), Mbunge wa Mbozi Magharibi, Godfrey Zambi (Kilimo, Chakula na Ushirika), Mbunge wa Mufindi Kusini, Mahmoud Ngimwa (Maliasili na Utalii) na Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo).
Waliopandishwa, kuhamishwa
Mbali na Dk Mahenge, Rais Kikwete pia amewapandisha manaibu waziri wengine watatu kuwa mawaziri kamili pasipo kuwahamisha wizara walizokuwa. Hao ni Saada Nkuya Salum anayekuwa Waziri wa Fedha, Lazaro Nyalandu (Maliasili na Utalii) na Dk Seif Rashid (Afya na Ustawi wa Jamii).
Balozi Sefue alisema Rais Kikwete amewahamisha aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuchukua nafasi ya Dk Nchimbi, wakati aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi amerejeshwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kuchukua nafasi ya Nahodha. Dk Mwinyi aliwahi kuongoza wizara hiyo.
Wengine waliohamishwa ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu kwenda kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, kuchukua nafasi ya Charles Kitwanga aliyehamishiwa Wizara ya Nishati na Madini kuendelea na wadhifa huo. Kitwanga anachukua nafasi ya George Simbachawene ambaye amehamishiwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima amehamishiwa Wizara ya Fedha kuchukua nafasi ya Janeth Mbene ambaye amehamishiwa, Wizara ya Viwanda na Biashara kuchukua nafasi ya Teu. Amos Makalla amehamishwa kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwenda Wizara ya Maji.
Sefue alisema mawaziri na manaibu waziri wapya wataapishwa leo saa 10 jioni Ikulu.

Hili ndilo Baraza la Mawaziri tunalolitaka

Baada ya kizaazaa cha wiki iliyopita ambapo mawaziri wanne walipoteza kazi zao kutokana na kuwajibishwa kwa vitendo vya ukatili na mauaji vilivyotokea wakati watendaji katika wizara zao walipokuwa wakiendesha ‘Operesheni Tokomeza Ujangili’ nchi nzima, kinachosubiriwa na wananchi hivi sasa ni Rais Jakaya Kikwete kuunda Baraza jipya la Mawaziri.
Kutokana na udhaifu mkubwa katika utendaji ambao kwa muda mrefu umeonyeshwa na mawaziri wengi katika Baraza la Mawaziri, hatudhani kama kuna mwananchi hata mmoja  anayemtarajia Rais Kikwete kujaza tu nafasi za mawaziri aliowafukuza wiki iliyopita.
Nderemo na vifijo vilivyotokana na furaha ya wananchi katika kila kona ya nchi baada ya mawaziri hao kuondolewa katika nyadhifa zao ni ishara tosha kwamba hawamtarajii Rais Kikwete kuishia hapo, isipokuwa kuwaondoa mawaziri wengine wengi ambao tayari wamethibitika na hata kutajwa na chama chao cha CCM kuwa ni ‘mawaziri mizigo’.
Hii bila shaka ni fursa nzuri kwa Rais Kikwete kusoma alama za nyakati, kwamba wananchi wamefika kikomo cha uvumilivu na sasa wamechoka na uzembe unaotokana na mawaziri dhaifu walio katika Baraza lake la Mawaziri. Hao ni  mawaziri ambao karibu muda wote wamekuwa nyuma ya matukio na kuishia kuwa watazamaji, huku shughuli za Serikali zikienda ndivyo sivyo kutokana na kutochukua hatua stahiki dhidi ya vitendo vya rushwa, uzembe, ubadhirifu wa fedha za umma na ufisadi uliokithiri.
Kutokana na mawaziri wengi kutokuwa na dhamira wala uwezo wa kuthubutu na kutenda, programu za Serikali kama ‘Kilimo Kwanza’ na ‘Matokeo Makubwa Sasa’ zimebakia kuwa vichekesho vya karne, pamoja na kuanzishwa kwa mbwembwe na fedha nyingi za walipakodi.
Ni bahati mbaya kwamba Rais Kikwete amebaki na muda mfupi mno kabla ya kumaliza kipindi chake cha uongozi Oktoba 2015. Kwa kifupi, amebakiwa na miezi 22. Kutokana na kuwapo programu nyingi ambazo hazijatekelezwa, anahitaji sasa kujipanga upya na kupata Baraza jipya la Mawaziri lenye watendaji waadilifu na wachapakazi. Baadhi ya wananchi wamekuwa wakielekeza lawama nyingi kwake kwamba uteuzi wake wa mawaziri kwa kiasi kikubwa umekuwa siyo wa umakini kwa maelezo kuwa, hauzingatii vigezo vya ufanisi na utumishi wa umma uliotukuka. Kwamba wengi wamekuwa ni mawaziri wa kufunga tai na kupeperusha bendera kwenye ‘mashangingi’ yao.
Tunakubaliana na wanaosema kwamba mawaziri wachapakazi katika Baraza lake wanahesabika katika kiganja cha mkono na kwamba Baraza hilo ni kubwa mno kupita kiasi. Jambo la kusikitisha ni kwamba ni mawaziri wasiozidi saba  wanaoweza kusimama leo na kuonyesha kitu walichokifanya na kukisimamia mpaka mwisho. Rais Kikwete atafanya vyema iwapo ataweka mfumo wa kupima utendaji wa mawaziri wake na kuwawajibisha wale wasiofikia viwango, badala ya kusubiri shinikizo la Bunge kama tulivyoshuhudia mwishoni mwa wiki.
Tunamshauri Rais Kikwete sasa aepuke kigezo cha ukanda na ukabila katika kuteua Baraza la Mawaziri. Hoja yetu ni kwamba siyo lazima kila kanda au mkoa kuwakilishwa na idadi sawa ya mawaziri hata kama baadhi yao hawana uwezo hata kidogo. Tunasema vigezo vikubwa katika uteuzi huo viwe ni uzalendo, uadilifu na utendaji, hata kama vigezo hivyo vitalazimu kuteuliwa mawaziri wawili kutoka katika kitongoji, kijiji au kata moja.