Sunday, 30 June 2013

CHADEMA NGANGARI,MBINU ZA CCM ZA GONGA MWAMBA

 KUIMARIKA kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kunazidi kuwachanganya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaotumia mbinu mbalimbali kukidhoofisha.
Tanzania Daima Jumapili imedokezwa kuwa licha ya viongozi wa CCM kuvitumia vyombo vya dola kuzima kasi ya CHADEMA, bado mambo yanaonekana kukiendea mrama chama tawala.
Hali ya mambo inaonesha kuwa CHADEMA inainyima usingizi CCM na serikali yake, ndiyo maana hivi sasa wameamua kukipaka matope kwa kutumia mbinu mbalimbali kuwafungulia kesi za ugaidi makada wao.
Uchambuzi wa kina wa matukio ya kisiasa ya hivi karibuni uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa kwa sasa CCM inakabiliwa na wakati mgumu kisiasa kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya chama hicho.
Kuna viashiria vya wazi kuwa enzi za CCM kutawala siasa za Tanzania zinaelekea ukingoni kadiri CHADEMA inavyoimarika.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa CCM imeamua kulitumia Bunge na vyombo vya dola, ikiwamo polisi kufanikisha azima yao ya kuidhoofisha CHADEMA.
Jeshi la Polisi limekuwa likituhumiwa na viongozi wa CHADEMA na wananchi kuwa linatumiwa kuanzisha vurugu zinazosababisha mikutano ya CHADEMA kuvurugika au kutokea vurugu.
Vurugu hizo zinaelezwa ni mipango maalumu ya kukipaka matope chama hicho kikuu cha upinzani nchini mbele ya umma ili wasikichague kwenye chaguzi zitakazofanyika mwakani na mwaka 2015.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wameanza kupata hofu juu ya mwenendo wa Jeshi la Polisi katika mikutano ya CHADEMA ambayo mara nyingi risasi na mabomu ya machozi hutumika.
Agosti 27, mwaka jana polisi walizuia na kuwatawanya wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wakielekea kwenye mkutano uliopigwa marufuku.
Katika purukushani hiyo kijana mmoja aliyekuwa akiuza magazeti mjini Morogoro aliuawa kwa risasi ingawa polisi walidai alipigwa na kitu kizito nyuma ya kichwa chake.
Septemba 2, jana mkoani Iringa, polisi walitumia mabomu ya machozi na risasi kukabiliana na wafuasi wa CHADEMA na mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, alilipuliwa na bomu. 
Viongozi na wanachama wa CHADEMA walikusanyika katika ufunguzi wa tawi la chama chao katika Kijiji cha Nyororo, mkoani Iringa.
Kumekuwapo juhudi za makusudi za polisi na CCM kujaribu kuihusisha CHADEMA katika matukio yote mawili ya mauaji kwa lengo la kukichafua lakini bado upepo unaonekana kuvuma vibaya kwa watawala na vyombo vya dola.
Tanzania Daima, Jumapili, limedokezwa kuwa mkakati wa pili unaotumiwa na CCM dhidi ya CHADEMA ni kuwabambikiza kesi za ugaidi viongozi wake ili chama hicho kionekane hakifai mbele ya Watanzania. 
Machi, mwaka jana, Mkururgenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare, alionekana kwenye mitandao ya kijamii akipanga kile kilichodaiwa na polisi na CCM kuwa mpango wa kumteka na kumdhuru Mhariri Mtendaji wa Mwananchi Communications, Denis Msacky.
Baadaye Lwakatare akashtakiwa mahakamani kwa tuhuma za ugaidi na kesi hiyo ikaanza kutumiwa kisiasa na makada wa CCM ili kuidhoofisha CHADEMA.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba, alikiri kufahamu watu walioiandaa video hiyo na kuiweka kwenye mitandao.
Kama ilivyokuwa kwa mipango mingine, mpango huu nao haukufua dafu baada ya Mahakama Kuu kumfutia Lwakatare mashtaka yote yaliyohusu ugaidi.
Kufutwa kwa mashtaka hayo kulikuwa pigo kubwa kwa CCM na polisi.
Harakati hizo zinaonekana kuzidi kushika kasi ambapo Juni 24 mwaka huu, makada wa CHADEMA wamefunguliwa mashtaka mengine ya ugaidi mkoani Tabora.
Makada hao wanatuhumiwa kumteka na kumdhuru kwa tindikali kada wa CCM wilayani Igunga mwaka 2011.
Washitakiwa hao ni pamoja na Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo, Evodius Justinian wa Bukoba, Oscar Kaijage wa Shinyanga, Seif Magesa Kabuta wa Mwanza na Rajab Daniel Kihawa wa Dodoma.
Watuhumiwa hao walisomewa shitaka la ugaidi kwa madai ya kumteka na kummwagia tindikali kada wa CCM, Musa Tesha, katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga uliofanyika mwaka 2011.
Juni 15, mwaka huu kulitokea mlipuko wa bomu katika mkutano wa CHADEMA wa kufunga kampeni za uchaguzi wa madiwani mkoani Arusha, ambapo watu wanne waliuawa na zaidi ya 70 kujeruhiwa.
Mara baada ya mlipuko huo viongozi wa CCM wamekuwa wakiihusisha CHADEMA na tukio hilo huku CHADEMA wakidai polisi na serikali ya CCM ndio wahusika wakuu.
Tukio hilo lilianza kuchukua mwelekeo wa kisiasa huku CCM wakionekana kutaka CHADEMA idhibitiwe katika mikutano yake ambayo imekuwa ikisababisha vifo na majeruhi.
Hata hivyo Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema wanao ushahidi unaomuonesha aliyerusha bomu alikuwa ni askari na alilindwa na wenzake wakati akitoka uwanjani hapo.
Katika mwendelezo wa kuibana CHADEMA kwa kuwafungulia makada wake kesi zisizo na msingi, juzi polisi walimshtaki mahakamani Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, kwa tuhuma za kumtukana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Polisi walidai kuwa Mbilinyi maarufu kama Sugu alisambaza katika mtandao wa kijamii wa facebook ujumbe wa kumtusi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, baada ya kauli yake kwamba: “Wanaokaidi amri ya polisi wapigwe tu,” kuwa ni upumbavu.
Hata hivyo, Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Dodoma ilitupilia mbali shtaka kutokana na hati ya mashtaka kukosa maelezo ya kutosheleza kuonesha kosa lililotendwa na Sugu, hivyo hati hiyo kukosa nguvu za kisheria.
Aidha, katika kuthibitisha kuwa viongozi wa CCM wamechanganywa na nguvu na ushawishi wa CHADEMA, uongozi wa Bunge nao umezidisha harakati zake za muda mrefu za kuwabana wabunge wa chama hicho kwa kuwazuia kuvaa suti za kombati ndani ya Bunge.
Kuzuiwa kwa mavazi hayo ambayo sasa yanatafsiriwa kuwa mavazi ya chama hicho, kunaelezwa ni ukiukwaji wa kanuni za Bunge.
Licha ya mbinu zote hizo, CHADEMA hivi sasa inaonekana kuimarika zaidi kwani katika uchaguzi wa udiwani uliofanyika hivi karibuni ilifanikiwa kuipoka CCM kata tatu.
Matokeo hayo yanatoa ishara kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa utaofanyika mwakani na ule mkuu utakaofanyika mwaka 2015, hali itakuwa ngumu zaidi kwa CCM.
Wadadisi wa masuala ya siasa wameweka wazi kuwa CCM imo katika hali ngumu kisiasa na haitashangaza kuiona ikishindwa vibaya katika uchaguzi mkuu ujao wa rais, wabunge na madiwani utakaofanyika mwaka 2015.
Kama CCM itashindwa katika uchaguzi mkuu ujao, basi itakuwa imefuata njia iliyopitwa na vyama vingine vikongwe katika Bara la Afrika, vilivyopigania uhuru wa nchi zao na ambavyo vimeondolewa madarakani na wanamageuzi kuanzia miaka ya 1990.
Vyama vikongwe Afrika vilivyowahi kuangushwa na wanamageuzi ni pamoja na chama kilichopigania uhuru wa Zambia cha UNIP chini ya Dk. Kenneth Kaunda, Chama cha Malawi Congress (MCP), kilichoongozwa na hayati Dk. Kamuzu Banda na Chama cha KANU kilicholeta uhuru wa Kenya, chini ya hayati Jomo Kenyata, ambacho kilitimuliwa madarakani mwaka 2002.

Monday, 3 June 2013

Familia ya Pistorius yashtushwa na picha





Familia ya mwanariadha mlemavu nchini Afrika Kusini, Oscar Pistorius, wameshstushwa na picha zilizofichuliwa za bafu alimomuulia mpenzi wake mnamo mwezi Februari.
Shirika la habari la Uingereza la Sky, mnamo Ijumaa, lilionyesha picha za kuogofya zinazoshukiwa kuwa za bafu ambalo mpenzi wa Pistorius Reeva Steenkamp, aliuawa.
Polisi walisema kuwa wamechukizwa mno na kufichuliwa kwa picha hizo.
Bwana Pistorius mwenyewe anakanusha madai ya kumuua mpenzi wake, kupitia mlango wa bafu alimokuwa , alisema alidhani kuwa alikuwa mwizi aliyevamia nyumba yake.
Anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa hatua ya mahakama mwanzo kutathmini kesi siku yake Jumanne.
Pistorius ni mwanariadha mlevamu asiye na miguu yake miwili ingawa hukimbia kwa miguu bandia au vyuma. Alishiriki michezo ya Olimpiki mjini London mwaka jana.
''Familia ya Pistorius ilimuunga mkono alipokuwa anajiandaa kufikishwa mahakamani , alisema mjomba wake,'' Arnold Pistorius.
''Tunaamini maneno yake , tunampenda na tutamuunga mkono kwa kila hatua ya kesi hii,''alisema Mjombake Pistorius.
"tumeshtushwa na picha hizi za ajali iliyotokea nyumbani kwa Oscar."
Msemaji wa polisi ameelezea kuwa polisi wanachunguza nani aliyefichua picha hizo .
''Kitendo hiki hakikuhitajika na kimetuudhi kweli. Hatujui picha hizi zimetoka wapi,'' alisema polisi huyo.
Pistorius atafikishwa mahakamani Jumanne kwa mara ya kwanza tangu kuachiliwa kwa dhamana, kufuatia kukamatwa kwake, kuhusu mauaji ya Steenkamp.
Kesi hiyo inatarajiwa kuakhirishwa kwani uchunguzi wa polisi ungali unaendelea.
Pistorius ameajiri baadhi ya mawaklili shupavu nchini Afrika Kusini kumtetea.
Anasema kuwa alimpiga risasi Bi Steenkamp kupitia mlango wa choo kimakosa baada ya kudhani kimakosa alikuwa mwizi.
Hata hivyo, viongozi wa mashtaka wanasema kuwa alimuua kwa maksudi baada ya wawili hao kugombana.

Gesi Mtwara yamtesa JK: Mawaziri watatu mashakani

MAANDAMANO makubwa ya kutaka Rais Jakaya Kikwete asikilize kilio cha wakazi wa Mtwara na Lindi wanaopinga ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam yanaandaliwa.
Baadhi ya wakazi wa Lindi na Mtwara kwa kushirikiana na Chama cha Wananchi (CUF), Juni 29 mwaka huu wanatarajia kufanya maandamano hayo kutoka makao makuu ya CUF Buguruni hadi Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Maandamano hayo pia yatakuwa na lengo la kumtaka Rais Kikwete awang’oe madarakani mawaziri watatu ambao ni Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Emanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani).
Wakizungumza katika mkutano wa kongamano la gesi lililowakutanisha wakazi wa Lindi na Mtwara, lililofanyika jana jijini Dar es salaam katika Ofisi za Makao Makuu ya CUF, baadhi ya wakazi hao walisema wamechoshwa na ahadi za serikali.
Walisema wanaamua kufanya maandamano kwenda Ikulu ili kilio chao kimfikie Rais Kikwete ambaye kama hatakisikiliza asitarajie wananchi watarudi nyuma kutetea rasilimali zilizoko mikoani mwao.
Walibainisha kuwa vurugu zilizotokea hivi karibuni mkoani Mtwara ni ishara ya kuchoshwa na mgawanyo wa rasilimali unaofanywa na serikali ambayo hivi sasa badala ya kuufikiria mkoa wa Mtwara unahangaika kujenga bomba la gesi kutoka mkoani humo.
Lipumba aanza
Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema vurugu zilizotokea hivi karibuni mkoani Mtwara zimesababishwa na serikali ya CCM iliyopuuza kilio cha umaskini cha wakazi cha mkoa huo.
Alisema serikali imeanza kushtuka na kwenda kuweka msingi wa ujenzi wa kiwanda cha saruji baada ya machafuko na upinzani kutoka kwa wananchi.
Alibainisha kuwa nguvu na kuwaziba midomo wanasiasa, wananchi na wanaharakati kamwe hazitoisaidia serikali kutatua mzozo huo unaoonekana kuutikisa utawala wa Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa watu wa Mtwara na Lindi wamekosa mahali na fursa za kuonana na viongozi wao kuzungumzia suala la gesi na matokeo yake imesababisha vurugu, manyanyaso kutoka kwa polisi waliokwenda kutuliza ghasia.
Profesa Lipumba alisema serikali inaeneza propaganda za uongo kwamba wananchi wa Mtwara hawataki Watanzania wengine wafaidi rasilimali zinazotoka katika mkoa huo.
Alisema wananchi wanataka maendeleo yaanzie katika mkoa huo kutokana na rasilimali zilizopo ndani yake ikiwemo kujengwa kiwanda cha mbolea na kiwanda cha kufua umeme wa MW 300 kama ahadi ya serikali ya mwaka 2011 inavyoeleza.
Aliongeza kuwa serikali katika ahadi zake miaka miwili iliyopita iliwaeleza wananchi wa Mtwara kwamba ingejenga kiwanda cha mbolea na kujenga kiwanda cha kufua gesi ambayo ingezalisha umeme wa MW 300 kisha uunganishwe kwenye gridi ya taifa lakini mipango hiyo haikufanyika.
Alisisitiza kwamba endapo mipango ya serikali iliyoainishwa kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ingetekelezwa hakuna vurugu wala matatizo ambayo yangejitokeza.
Alisema wananchi wanaoishi mikoa ya kusini wanadharaulika na kuonekana hawastahili kupata haki kama watu wa mikoa mingine na kwamba hali hiyo imewafanya wachoke na kufanya matendo ambayo yataaonyesha kuchoshwa na kuhitaji mabadiliko.
Wakazi wafunguka
Baada ya Lipumba kuzungumza, wakazi waliokuwapo ukumbini hapo walipata fursa ya kutoa dukuduku ambapo wengi wao walitaka mawaziri watatu wang’olewe madarakani.
Waziri Nchimbi anatakiwa kung’olewa kwa sababu ya kutowachukulia hatua polisi waliokwenda kutuliza ghasia mkoani humo kuendesha vitendo vya kihalifu, kubaka na kuwanyanyasa wananchi.
Mmoja wa wakazi hao alisema Nchimbi alisema damu ya polisi iliyomwagika haitapotea bure wakati askari hao walikufa kwenye ajali wakiwa njiani kwenda Mtwara.
“Polisi hawakufa kwenye mapambano, walikufa kwa ajali ya gari lao sasa wananchi watalipa vipi vifo hivyo? Waziri Nchimbi alichemka na hatufai,” alisema mkazi huyo.
Pia wananchi hao walimtaka Waziri Shamsi Vuai Nahodha aondolewe madarakani kwa kushindwa kuulinda mkoa huo pamoja na kutowawajibisha wanajeshi waliokiuka maadili ya kazi zao wakati wakilinda usalama mara baada ya kutokea kwa vurugu.
Mwananchi mwingine alitaka Waziri Muhongo aondolewe kwa kuwa ameshindwa kusimamia suala hilo la gesi lililo chini ya wizara yake na hivyo kusababisa vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.