Pembezoni mwa Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Tanzania (Tec),
ujenzi unaendelea wa barabara na daraja la kuunganisha Mji wa Kigamboni
na Jiji la Dar es Salaam, eneo la Mkondo wa Kurasini. Ujenzi huo
unafanywa na kampuni mbili kutoka nchini China.
Kampuni hizo ni; China Railway Jiangchang (T) Ltd
na China Major Bridge, mradi ambao unatarajiwa kukamilika Januari 2015
ukigharimu dola 136 milioni za Marekani, fedha ambazo asilimia 60
zinatolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kiwango
kingine kinalipwa na serikali.
Ujenzi huo unafanyika ikiwa ni sehemu ya
kuwaondolea kero ya Kivuko wakazi wapatao 679,291 sawa na asilimia 5.7
ya watu wote wa Dar es Salaam na idadi hiyo ni tofauti na mamia wengine
ambao wanaenda eneo hilo kila siku kwa ajili ya shughuli tofauti
zikiwamo za kiuchumi.
Eneo la Kigamboni ambalo limelengwa kuwa mji mpya
wa kisasa, lina utajiri mkubwa wa mazao mbalimbali ya chakula, biashara
kama vile mbogamboga, matunda, viazi vitamu, magimbi, nazi, korosho na
mazao ya baharini wakiwamo samaki, mapambo ya majumbani na bidhaa
nyingine.
Pia mji huo una hifadhi historia kwani maeneo ya
Mbwamaji, Puna, Kimbiji, Pembamnazi, Buyuni na kwingineko kuna mabaki ya
majengo ya kihistoria ambayo hata hivyo yanatoweka kutokana na utunzaji
na harakati za ujenzi wa nyumba za kisasa.
Pia eneo hilo linasifika kwa kuwa na fukwe zenye
mchanga wa kuvutia na mandhari nzuri za kupendeza hali ambayo inachangia
kuwavutia watalii na wageni wengine wanaotembelea eneo hilo ambalo pia
upande mwingine ina hazina kubwa ya jiwe la jasi ambalo hutumika
kutengenezea saruji.
Kulingana na mkandarasi ambaye ni mbunifu wa mradi
huo ambalo ni la kuning’inia (Cable-Stayed Bridge), lina urefu wa mita
680 na upana wa mita 27.5 na linatarajiwa kuwa mbadala wa Kivuko cha
Kigamboni ambacho kina pantoni za Mv Kigamboni na Magogoni.
Ujenzi huo unakaribia kukamilika, lakini hadi sasa
gharama za kulitumia daraja hilo kwa wananchi wa kawaida, wenye magari,
baiskeli, mikokoteni na vyombo vingine bado hazijainishwa. Suala hilo
linawaacha watu weni katika maswali mengi kuliko majibu.
Ingawa hakijatajwa kiwango kitakachokuwa kinatozwa
kama ada na ushuru mwingine, lakini bado kuna utata iwapo mradi huo
utakamilika kwa wakati kutokana na sababu nyingi ikiwa ni pamoja na
ukweli kuwa mradi umefikia zaidi ya asilimia 50 ya ujenzi wake, lakini
kuna utata iwapo ujenzi utakamilika kwa wakati.
Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa hadi hivi sasa
serikali haijatoa kiasi chochote kati ya asilimia 40 ya fedha ambazo
wanatakiwa kuchangia ili kukamilisha mradi huo hali ambayo inadaiwa
kukwamisha upatikanaji wa fedha za fidia kwa baadhi ya watu ambao
wanaguswa na mradi.
Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Karimu Mataka wa
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), anakiri serikali kutokutoa
fedha ambazo iliahidi hadi sasa, na hali hiyo imechangia mradi kushindwa
kukamilika Januari mwakani kama ilivyokadirwa na badala yake sasa
unatarajiwa kukamilika Juni mwakani.
John Ngoma maarufu kwa jina la Jitu,mkazi wa eneo
la Kijibweni ambaye eneo lake limechukuliwa kwa ajili ya kutoa nafasi ya
utekelezaji wa mradi huo anasema ni vizuri wakaelezwa kiasi cha fidia
watakachopewa kabla ya uthamini kufanywa jambo ambalo linapingwa na
mfumo mzima wa fidia.
Kulingana na taratibu na kanuni za fidia, zinafanyika kwanza,
kisha ndio malipo hupangwa tofauti na wanavyotaka wakazi hao ambao
wanataka waambiwe kwanza watalipwa nini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Injinia Mussa
Iyombe, alipotembelea kujionea maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo,
anasema lilitarajiwa kukamilika Januari mwaka 2015, lakini sasa itaenda
hadi Juni na wakazi wa eneo hilo ambao anasema idadi yao haizidi watu
wanne suala lao limefikishwa wizarani.
Anasema ujenzi wa daraja hilo ulitarajiwa
kukamilika Januari mwakani, lakini kutokana na changamoto walizokutana
nazo wahandisi chini ya bahari na kwa wananchi zimewafanya wachelewe na
sasa wanatarajia kukamilisha kazi hiyo Julai mwakani.
Mhandishi anasema kuwa licha ya changamoto zote
wakandarasi wamekuwa wakiendelea vizuri na kile ambacho kimefanyika hadi
hivi sasa kinatoa matumaini kwa Watanzania kuwa mradi utakamilika kwa
wakati hivyo kuwaondolea kero.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Vijibweni, Bahari
Mohamed anasema kimsingi fedha za fidia kwa ajili ya watu hao ambao
wamegoma kutoa nafasi kwa mradi zipo na iwapo wataridhia na kuvunja
nyumba zao watalipwa na iwapo wataendelea na mgomo huenda nyumba hizo
zikavunjwa kwa nguvu na fidia wataifuata wakitaka.
“Fedha zipo isipokuwa wamegoma watu watatu katika
eneo ambako wamejenga nyumba, mmoja wao anamiliki kiwanja ambacho
hakijaendelezwa,” anasema Mohamed.
Mohamed anasema daraja litakuwa na faida kiuchumi iwapo wakazi wake watalitumia vizuri na kuwekwa utaratibu wa kueleweka.
Anasema ingawa hajui watu watatozwa kiasi gani cha
fedha wakati wa kuvuka, amedokezwa kwamba waenda kwa miguu watapita
bure isipokuwa wale wenye vyombo vya usafiri kama vile pikipiki, magari
na mikokoteni.
“Nasikia waenda kwa miguu itakuwa bure hilo halina uhakika kwani hadi sasa haijaelezwa gharama zake zitakuwa vipi,” anasema.
Mmoja wa wachukuzi wa abiria katika boti iitwayo
Kilimanjaro katika eneo hilo, Idrissa Hussein anasema wao wataangalia
upepo unavyoeenda kwani wamekuwa wakitoa huduma hiyo kwa kipindi kirefu
tena katika mazingira magumu.
“Kama watatoza fedha watu kuvuka tutaangalia ni
kiasi gani kama italipa tutaendelea na huduma kwa kiwango cha sasa au
pungufu yake la sivyo tutaangalia jambo lingine la kufanya kwani mashine
na vyombo bado ni mali yetu,” anasema.
Mkazi wa eneo hilo, Jonathan Ngosha anasema endapo
daraja hilo litatumika kutoa huduma kwa wananchi, litakuwa ni msaada
mkubwa kwao.
Lakini anasema Daraja la Kigamboni likitumiwa kama kitegauchumi,
watu wengi wataendelea kutumia boti kuvuka kutoka Kigamboni hadi upande
wa pili wa maeneo ya Kurasini.
Mkazi huyo anataka gharama za matumizi ya daraja
hilo ziwe wazi kwa ajili ya kuwaandaa wakazi wa eneo hilo na sio kuwa
kimya kama ilivyo sasa kwani hali hiyo inazua maswali mengi kuliko
majibu.

No comments:
Post a Comment